2 Samuel 8

Ushindi Wa Daudi

(1 Nyakati 18:1-17)

1 aBaada ya muda, Daudi akawashinda Wafilisti na kuwatiisha, naye akautwaa Metheg-Amma kutoka mikononi mwa Wafilisti.

2 bPia Daudi akawashinda Wamoabu. Akawafanya walale chini kwa mstari akawapima kwa urefu wa kamba. Kila alipopima urefu wa hiyo kamba mara mbili hilo kundi waliuawa na alipopima mara ya tatu aliwaacha hai. Kwa hiyo Wamoabu wakawa chini ya Daudi nao wakamletea kodi.

3 cZaidi ya hayo, Daudi akapigana na Hadadezeri mwana wa Rehobu, mfalme wa Soba, alipokwenda kurudisha tena utawala wake kwenye eneo la Mto Frati. 4 dDaudi akateka magari yake ya vita 1,000, askari wapanda farasi 7,000 na askari 20,000 watembeao kwa miguu. Daudi akawakata wale farasi wote wakokotao magari mishipa ya miguu, isipokuwa farasi 100 hakuwakata.

5 eWaaramu wa Dameski walipokuja kumsaidia Hadadezeri mfalme wa Soba, Daudi akawashambulia na kuwaua 22,000 miongoni mwao. 6 fDaudi akaweka askari walinzi katika ufalme wa Waaramu huko Dameski, nao Waaramu wakawa watumwa wake na kumlipa ushuru. Bwana akampa Daudi ushindi kote alipokwenda.

7 gDaudi akazitwaa ngao za dhahabu zilizokuwa za maafisa wa Hadadezeri na kuzileta Yerusalemu. 8 hKutoka miji ya Beta
Beta ulikuwa mji wa Aramu-Soba ambao uliitwa Teba kwa Kiaramu; pia uliitwa Tibhathi ( 1Nya 18:8 ).
na Berothai, iliyokuwa miji ya Hadadezeri, Mfalme Daudi akatwaa shaba nyingi sana.

9 jTou, mfalme wa Hamathi, aliposikia kwamba Daudi amelishinda jeshi lote la Hadadezeri, 10akamtuma mwanawe Yoramu kwa Mfalme Daudi kumsalimu na kumpongeza kwa ushindi wake katika vita dhidi ya Hadadezeri, kwa kuwa Hadadezeri alikuwa amepigana vita na Tou. Yoramu akamletea Daudi vyombo vya fedha, dhahabu na shaba.

11 kMfalme Daudi akaviweka vifaa hivi wakfu kwa Bwana, kama vile alivyokuwa amefanya kwa fedha na dhahabu kutoka kwa mataifa yote aliyokuwa ameyashinda: 12 lyaani Edomu, Moabu, Waamoni, Wafilisti na Waamaleki. Pia akaweka wakfu nyara alizoteka kutoka kwa Hadadezeri mwana wa Rehobu, mfalme wa Soba.

13 mNaye Daudi akapata sifa baada ya kurudi kutoka kuwaua Waedomu 18,000 katika Bonde la Chumvi.

14 nAkaweka kambi za askari walinzi katika Edomu yote, nao Waedomu wakawa chini ya Daudi. Bwana alimpatia Daudi ushindi kila alipokwenda.

Maafisa Wa Daudi

15 oDaudi akatawala Israeli yote, akitenda lililo haki na sawa kwa watu wake wote. 16 pYoabu mwana wa Seruya alikuwa jemadari wa jeshi; Yehoshafati mwana wa Ahiludi alikuwa mweka kumbukumbu; 17 qSadoki mwana wa Ahitubu na Ahimeleki mwana wa Abiathari walikuwa makuhani; Seraya alikuwa mwandishi; 18 rBenaya mwana wa Yehoyada alikuwa msimamizi wa Wakerethi na Wapelethi; nao wana wa Daudi walikuwa washauri wa mfalme.
Copyright information for SwhKC